Na MWANDISHI WETU
Ijumaa, Juni 6, 2025
WAREMBO wa Kahawa Queens wiki hii wameazimia kujituma kwa udi na uvumba wahakikishe wamelipiza kisasi kwenye mechi za Nairobi East Regional League (NERL). Kahawa Queens ya kocha Hussein ‘Machinga’ Mohamed itateremka dimbani kukaribisha Kariobangi All Starlets ugani Kahawa Barracks, Nairobi, Jumapili, Juni 8, 2025.
Nayo Dadstar ya kocha Peter Aloo itapepetana na viongozi wa kipute hicho Embakasi South Ladies ugani Tom Mboya, huku Fearless Starlets ikizuru Kariobangi Primary kukabili Kariobangi Sharks Women. Hata hivyo meneja wa Kahawa Nelly Kwamboka anakiri kuwa wanatarajia mtihani mgumu mbele ya wapinzani wao lakini wapo imara kuwakabili.
“Tuna imani tuna mboga kuwaweka chini wapinzani wetu ili kulipiza kisasi baada ya kupigwa wiki iliyopita,” alisema na kuongeza kuwa kipute hicho kinashuhudia upinzani mkali kinyume na matarajio ya wengi. Kwenye mechi za wiki iliyopita, Kahawa iliangukia pua ilipoduwazwa kwa magoli 5-0 na Embakasi South Ladies.
Kahawa inategemea huduma za wachezaji wepesi kama Mejumaa Kombo, Joan Chepkoech, Shango Doreen, Lillian Shamala na Susan Oduor kati ya wengine. “Tutakuwa mbioni kupigania alama tatu muhimu kama tulivyofanya wiki iliyopita,” alisema kocha wa Dadstar na kuonya wachezaji wake kamwe kutodharau wapinzani wao. Dadstar itategemea huduma za chipukizi shupavu kama Everlyne Nthenya na Mary Akinyi kati ya wengine. Dadstar itashuka dimbani ikijivunia kuzoa ushindi wa magoli 2-0 mbele ya Acofoa Starlets wiki iliyopita.
Kwenye mfululizo wa ratiba hiyo, makocha Arnold Otieno na Mark Arnold wataongoza MAS Queens, kukabili Soweto Starlets ugani Muhuri Muchiri. MAS Queens inalenga kubeba alama tatu huku ikijivunia kuzaba Fearless Ladies kwa magoli 5-1 wiki iliyopita. Nayo Kamongo Starlets itachuana na Acofoa Starlets, Mrembo Ladies itapepetana na Kahawa Pride Lionesses, Bright Future Starlets itakwaruzana na Shrink Pack Starlets, huku Kayole Starlets ikivaa Mukuru Talent Academy.
Post Views: 189