Na RIPOTA WETU
Alhamisi, Machi 13, 2025
ZIARA ya rais William Ruto na Naibu wake Prof Kithure Kindiki, jijini Nairobi, Jumatano, katika eneo Bunge la Dagoretti kusini na Westlands ilikuwa ya kufana. Rais alisema kuwa serikali yake itaajiri vijana 40,000 katika mradi wa kuzoa taka kwenye mto Nairobi, kuweka mazingira safi ili kuvutia wawekezaji nchini.
Vijana watapewa jukumu la kuweka mazingira safi, ujenzi wa mabomba ya maji taka na ujenzi wa nyuma za bei nafuu. Wakati huu wapo vijana 22000 katika mitaa ya Kaunti ya Nairobi wakipiga shughuli hizo kupitia agizo la Rais Ruto. Pia wengine wapatao 18,000 watapewa ajira hiyo na baadaye wengine 1000 watafuata mkondo huo.
Wakati wa ziara hiyo eneo la Dagoretti na Westlands, Naibu Rais Prof Kithure Kindiki aliwahimiza vijana wajisajili upesi kwa mradi huo wa miaka miwili akidai utawapa mwongozo wa kimaendeleo.
“Tungetaka wavulana na wasichana wapate ajira ili waweze kujikimu kimaisha huku tukiendesha nchi mbele,” alisema Pro Kindiki. Aliongeza kuwa wamepania tuwe na serikali ya uzalendo, umoja, ili kujenga Taifa lenye mshikamano,” alifafanua Naibu Rais.. Hata hivyo, Rais Ruto alihakikishia wananchi kwamba Bima ya afya ya SHA, itafanyiwa marekebisho mara moja ili ifaidi kila mwananchi bila ubaguzi. “Hapo awali Bima ya matibabu ilinufaisha wanaofanya kazi na wenye Pesa, lakini wakati huu, tutahakikisha kila mwananchi anapata matibabu ,” akasema Rais. Wakati huo pia alihaidi Gavana wa Kaunti ya Nairobi, Johnson Sakaja kuwa hospitali iliyokwama kukamilika eneo ya Dagoretti kusini, iliyotarajia kugharimu Sh 230 milioni itakamilishwa hivi karibuni. Aliamuru wajenzi wa hospitali hiyo waanza kazi baada ya wiki mbili bila kuchelewa. Aliagiza pia ujenzi huo ung’oe nanga mwezi Aprili hadi Agosti, 2025 ili iwe imekamikika.
Naye Naibu Rais, alisema wanatarajia kujumuisha vijana wapatao 22,000 katika miradi tofauti kama mtandao ICT na mradi wa ajira katika mataifa ya ng’ambo ili wajiendeleze kimaisha. Rais alisema miradi wa soko ya kisasa ya Riruta na hospitali ya Dagoretti itapewa kipau mbele na serikali yake. Rais alidokeza kuwa serikali imo mbioni kuona kwamba Shule ya Msingi ya Kawangware pia sekondari ya Gatina eneo la Westlands, shule ya Msingi ya Kangemi na Daraja la Kangemi zitashughulikiwa upesi. Alidokeza kuwa kuungana pamoja na wananchi ni muhimu kwa manufaa ya umoja wa nchi.
