Na RIPOTA WETU
Jumamosi, Januari 11, 2025
SHULE ya Upili ya Thika High inajivunia wanafunzi wapatao 25 kuandikisha alama za A na A- kwenye mtihani wa kitaifa wa KCSE mwaka 2024. Wanafunzi wa shule hiyo inayopatikana katika Kaunti ya Kiambu, wanasherekea ushindi huo unaotajwa kama ufanisi wa kila mmoja shuleni.
Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Bw Julius Muraya anasema ushindi huo umechangiwa pakubwa na ushirikiano wa walimu, wanafunzi na wazazi. Alitaja vigezo tatu muhimu vilivyosaidia ufanisi wa shule hiyo kama uwezo wake Mungu, nidhamu na wanafunzi kutia bidii masomoni.
”Wazazi walichangia pakubwa kupitia kulipia wanao karo na kuwapa motisha kutia bidii kwa kusoma. Nashukuru sana kila mmoja aliyehusika kwa njia moja ama nyingine kwenye juhudi za kuhakikisha tumepiga hatua kwenye mtihani huo,” anasema mwalimu huyo.
Kwa jumla wanafunzi wa Thika High wapatao 355 walipata alama ya C+ na zaidi. Ni dhahiri shahiri kuwa wanafunzi hao wote wana nafasi ya kujiunga na vyuo vikuu. Ibrahim Chacha aliyezoa alama ya A alikuwa mwenye furaha tele huku akinyanyuliwa juu juu na wanafunzi wenzake mnamo Ijumaa, Januari 10, 2024 walipokuwa wanasherekea ufanisi wa Shule hiyo kwenye mtihani huo.
”Kiukweli ni kwa uwezo wake Mungu nimefanya vizuri maana haikuwa rahisi bali nilijitolea mhanga kwa masomo. Nashukuru Mola kwa kunipa uwezo wa kupata mafanikio hayo,” alisema Chacha. Aliongeza kuwa ana furaha tele kwa ufanisi huo ambapo sasa anasubiria kujiunga na Chuo Kikuu anakopania kusomea Udaktari.
Mwanafunzi mwingine aliyepata alama A- , Francis Kagiri alisema alijinyima usingizi kwa muda mrefu maana wakati mwingi alikuwa akiamka na wenzake saa 9 za alfajiri! kuanza kusoma. Mwanafunzi Prince Mugonyi pia aliyepata alama ya A- alisema masomo ya alfajiri ndiyo yamechangia kuzalisha matunda mema. “Ingawa natamani kuwa mchora ramani ya ujenzi naomba serikali ipunguze ada ya vyuo vikuu ili kila mwanafunzi apate afueni ya kugharamia elimu ya Chuo Kikuu,” akasema Mugonyi.
Mwalimu huyo alisema kwamba wanafunzi 50 wametokea familia fukara ambapo wameachia Shule deni la takriban Sh1.9 milioni. ”Natoa wito kwa wahisani popote walipo wajitokeze angalau kulipia wanafunzi hao deni hilo maana wazazi wengi wanapitia hali ngumu kifedha,” akasema Bw Muraya. Anatoa wito kwa serikali angalau ipunguze ada ya vyuo vikuu kwa kiwango kinachowapa wazazi nafasi ya kulipa kirahisi.
Post Views: 510